Klabu yetu imeingia mkataba wa miaka miwili na Kampuni ya Emirate Aluminium ACP wenye thamani ya Sh milioni 300 kwa ajili ya kutoa motisha kwa wachezaji kila mwezi.
Msimu uliopita kupitia Emirate Aluminium Profile ilikuwa inatoa Sh milioni moja kila mwezi kwa mchezaji bora wa mwezi lakini leo wamekuja na Emirate Aluminium ACP lengo likiwa lile lile motisha kwa wachezaji.
Mtendaji Mkuu wa klabu, Barbara Gonzalez amesema Emirate Aluminum imeona faida inayopatikana kwa kutangaza na klabu yetu hivyo kwa pamoja tumekubaliana kuingia mkataba huo.
Barbara ameongeza kuwa ni jambo zuri kumpa motisha mchezaji kila anapofanya vizuri na ameipongeza Emirate Aluminium ACP kwa kuliona hilo na kulitekeleza kwa faida ya timu ambayo kila mmoja ameona.
“Leo tumeingia mkataba wa miaka miwili na Emirate Aluminium ACP ambapo msimu uliopita walikuwa wanafanya majaribio na wameona faida yake ndiyo maana wamekuja tena,” amesema Barbara.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Emirate Aluminium, Deogratius Marandu amesema ameona faida ya kufanya kazi na Simba kutokana na mauzo yao sokoni kuwa makubwa kwa muda wote waliokuwa wanafanya kazi nasi.
“Simba ni bingwa kwa upande wa uwanja nasi tunataka kuwa mabingwa kupitia bidhaa zetu za Emirate Aluminium ACP ndiyo maana tuko hapa leo kusaini mkataba huo,” amesema Marandu.