Kikosi cha timu yetu ya Wanawake ya Simba Queens mchana huu kimefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Gymkhana kujiandaa na mchezo wa tatu wa Kundi A wa michuano ya Cecafa Samia Women Cup dhidi ya FAD FC.
Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Moi Kasarani saa saba mchana na ndiyo sababu kikosi chetu kimefanya mazoezi mchana huu ili kuendana na mazingira ya kesho.
Maandalizi kuelekea mchezo wa kesho yamekamilika kwa asilimia kubwa na wachezaji wapo kwenye hali nzuri na tayari kuwakabili FAD FC.
Nahodha wa kikosi chetu, Violeth Nicholaus amesema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo na wamejipanga kuwapa raha mashabiki wetu huku akiwaomba kutuombea kwa Mungu ili tufanye vizuri.
Timu yetu ya Simba Queens inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi A ikiwa na alama nne sawa na vinara Lady Doves ya Uganda lakini ikitofautiana uwiano wa mabao.