Ushindi wa mabao 2-0 tuliopata leo dhidi ya Coastal Union, umetufanya kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu 2020/21 kwa mara ya nne mfululizo.
Katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Kocha Didier Gomes alifanya mabadiliko ya wachezaji watano ambapo tulihitaji alama moja pekee ili kuwa mabingwa lakini ushindi huo umetuhakikishia nafasi nzuri zaidi.
Nahodha John Bocco alitufungia bao la kwanza dakika ya 13 kwa mpira wa adhabu ndani ya 18 kufuatia mlinda mlango wa Coastal, Abubakar Abas kurudishiwa mpira na mlinzi wake na kuudaka.
Chris Mugalu alitupatia bao la pili dakika ya 23 baada ya kupokea pasi ya David Kameta kabla ya kumpiga chenga mlinda mlango wa Coastal na kuweka kimiani.
Sasa tumefikisha pointi 79 alama tisa juu ya wanaoshika nafasi ya pili huku tukiwa na mechi mbili mkononi.
Kocha Gomes aliwatoa Bocco, Clatous Chama na Mugalu na kuwaingiza Medie Kagere, Said Ndemla na Hassan Dilunga.