Katika mchezo wetu wa watani wa jadi wa kesho tutakosa huduma ya nyota wetu wawili Ibrahim Ajibu ambaye anasumbuliwa na Malaria pamoja na Jonas Mkude ambaye suala lake la kinidhamu bado halijamalizika.
Pamoja na uwezo na umuhimu wa nyota hawa kuelekea mchezo wa kesho lakini bado wengine walio fiti watahakikisha tunashinda na kutwaa ubingwa wetu kwa mara ya nne mfululizo.
Kocha Msaidizi Seleman Matola amesema maandalizi yamekamilika na wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mchezo ukiacha hao wawili ambao amewataja.
“Maandalizi yamekamilika wachezaji wako vizuri na morali ipo juu, tutawakosa Ajibu na Mkude lakini wengine wote wapo tayari na tunaamini tutashinda na kutetea ubingwa wetu,” amesema Matola.
Kwa upande wake nahodha msaidizi, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema wao kama wachezaji wamejiandaa vizuri na wapo tayari kufuata maelekezo watakayopewa na makocha na kuyafuata uwanjani.
“Tumetoka kucheza mechi kubwa dhidi ya Azam na kesho tunacheza kubwa nyingine, tumejipanga vizuri na tunajua utakuwa mchezo mgumu lakini tupo tayari,” amesema Zimbwe.
2 Responses
simba mnyama lazima amkalishe yanga kesho 🦁🔥💥
Furaha yangu leo ni kumfunga utopolo tu