Gomes analitaka taji la FA, aizungumzia Azam

Kocha Mkuu Didier Gomes, ameweka wazi kuwa mchezo wetu wa kesho wa Nusu Fainali ya Michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Azam FC utakuwa mgumu lakini itakuwa ngumu kwao kutuzuia kuingia fainali.

Gomes amesema malengo yetu tangu tunaanza msimu huu ilikuwa ni kutetea taji hili pamoja na ligi kuu ambalo tuna asilimia kubwa ya kulinyakua tena kwa mara ya nne mfululizo.

“Tangu mwanzo wa msimu lengo letu lilikuwa ni kutetea taji hili na sasa tumefika hatua hii kwa hiyo tumejipanga kushinda na kuingia fainali.

“Azam ni timu nzuri na tunakumbuka mchezo wa mwisho tulipokutana tulifanikiwa kumiliki mchezo ila tulipoteza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza lakini tumejitahidi kuondoa mapungufu ili kupata ushindi,” amesema Kocha Gomes.

Aidha, Kocha Gomes amewashukuru wapenzi wa soka hapa Songea kwa mapokezi makubwa waliyotupa wakati tumewasili na tunajiandaa kuwalipa kwa ushindi kwenye mchezo wa kesho.

Kwa upande wake Nahodha John Bocco amesema kwa upande wa wachezaji hali zao ziko sawa na morali ipo juu ambapo matumaini ya ushindi ni makubwa kesho.

“Sisi kama wachezaji tupo tayari kwa mchezo, morali ipo juu na tutafuata malekezo tutakayopewa na makocha wetu. Azam ni timu bora tunaiheshimu lakini tumejipanga kushinda,” amesema Bocco.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER