Leo saa mbili usiku kikosi chetu kitashuka katika uwanja Obedi Itani Chilume nchini Botswana kuikabili Gaborone United katika mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Huu ni mchezo wetu wa kwanza kwenye michuano hii mikubwa barani Afrika ambao malengo yetu ni kupata matokeo chanya.
Wachezaji wote 22 tuliosafiri nao wapo kwenye hali nzuri na jana wamefanya mazoezi ya mwisho kujiweka sawa na hakuna aliyepata majeraha yatakayomfanya kuukosa mchezo wa leo.
Kauli ya benchi la ufundi
Kocha Mkuu Fadlu Davids ameweka wazi kuwa haitakuwa mechi nyepesi kutokana na Gaborone kuwa Mabingwa wa nchi huku wakiwa na faida ya kucheza nyumbani ingawa haitakuwa changamoto kwetu kwakuwa tuna uzoefu mkubwa.
Fadlu ameongeza kuwa tuna kikosi imara cha ushindani ambacho kinaweza kutupa matokeo chanya huku akiweka wazi mechi mbili za ushindani tulizopata za Simba Day na Ngao ya Jamii zimezidi kutuimarisha.
“Kwenda hatua ya makundi unahitaji kushinda mechi zote nyumbani na ugenini na sisi tumejiandaa kufanya hivyo. Timu yangu imecheza mechi mbili zenye uzito mkubwa Simba Day na Ngao ya Jamii kwahiyo wachezaji wangu wapo tayari kwa ushindani.” amesema Fadlu.
Wachezaji wapo kamili asilimia 100
Nahodha wa timu, Shomari Kapombe amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri kwa asilimia 100 kuhakikisha wanapambana hadi mwisho kuisadia timu kupata matokeo chanya.
“Haitakuwa mechi rahisi lakini kwa upande wetu kama wachezaji tupo tayari kujitoa, kila atayepata nafasi ya kucheza atahakikisha anaisaidia timu kupata,” amesema Kapombe.
Watatu wanatumikia adhabu
Kocha Msaidizi, Darian Wilken na Kocha wa viungo, Riedoh Berdien hawatakuwa sehemu ya benchi letu la ufundi kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu waliopata katika mchezo wa fainali ya mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane uliopigwa Uwanja wa New Amaan, Zanzibar Mei 25/2025.
Kiungo mkabaji Yusuph Kagoma nae alionyeshwa kadi nyekundu na amebaki Dar es Salaam hivyo hatakuwa sehemu ya mchezo wa leo.
Bajaber na Hamza ni majeruhi
Kiungo mshambuliaji, Mohamed Bajaber ataendelea kukosekana kwenye mchezo wa leo kutokana nakuwa majeruhi pamoja na mlinzi wa kati Abdulrazak Hamza ambaye alipata majeraha kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.