Fadlu: Nimeridhika na Kikosi nilichonacho

Kocha Mkuu, Fadlu Davids ameweka wazi kuwa ameridhika na kikosi chetu kuelekea kuanza kwa msimu mpya wa mashindano 2025/2026.

Fadlu amesema msimu uliopita ulikuwa ni kwa ajili ya kujenga msingi wa kikosi lakini huu unaoanza tupo na timu imara ambayo tunaweza kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani na nje.

Fadlu ameongeza kuwa ili kuwa timu bora Afrika kama zilivyo Mamelodi Sundowns na Al Ahly tunahitaji madirisha matatu mpaka manne ya usajili lakini kikosi tulichonacho kuelekea msimu mpya wa mashindano kipo imara na tayari kwa mapambano.

“Tunategemea kuwa na msimu mzuri zaidi ya uliopita, tumefanya usajili mzuri kwenye kila eneo na baada ya juzi dirisha la usajili kufunga nimeridhika na aina ya kikosi nilichonacho,” amesema Fadlu.

Akizungumza kama atawapa nafasi wachezaji waliopo kwenye majukumu ya timu ya Taifa kwenye mchezo wa kesho wa Simba Day dhidi ya Gor Mahia, Fadlu amesema “Itategemea kama wataanza na kucheza dakika 90 leo dhidi ya Niger kesho tutawapumzisha ili kuwalinda na majeraha.”

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, kiungo mshambuliaji, Mohamed Bajaber amesema kila mmoja yupo tayari kujitoa kwa ajili ya kuhakikisha Wanasimba wanafurahi kwenye siku yetu muhimu.

“Tunafahamu hii ni mechi ya kirafiki lakini Simba kila mchezo ni mkubwa kwetu. Tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri hasa tukijua mashabiki wetu watakuja kwa wingi,” amesema Bajaber.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER