Kikosi chetu kimeibuka na ushindi wa bao moja dhidi ya Al Zulfi inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza nchini Saudi Arabia kwenye mchezo wa kirafiki.
Mchezo huo ulianza kwa timu zote zikishambuliana kwa zamu lakini zikiwa makini kuhakikisha wanakuwa salama muda wote.
Kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua alitupatia bao hilo pekee kwa mpira wa adhabu uliotinga wavuni moja kwa moja dakika ya 24 baada ya Semfuko kufanyiwa madhambi nje ya 18.
Wakati timu zikirejea baada ya mapumziko kocha Fadlu Davids alifanya mabadiliko ya wachezaji nane ambao ni Alexander Erasto, David Kameta, Rushine De Reuck, Anthony Mligo, Saleh Karabaka, Awesu Awesu, Steven Mukwala na Joshua Mutale.
Al Zulfi walifanya mashambulizi kadhaa langoni kwetu lakini hata hivyo safu ya ulinzi ilikuwa imara muda wote kuhakikisha tunakuwa salama.
Katika mchezo huo wachezaji wote wamepata nafasi ya kucheza ili kuendelea kuwa tayari kuelekea msimu mpya wa mashindano.