Tupo tayari kuikabili Kagera Sugar

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa KMC Complex kuikabili Kagera Sugar kwenye mchezo wa mzunguko wa 30 wa Ligi Kuu ya NBC.

Licha yakuwa Kagera imeshuka daraja lakini inabaki kuwa moja ya timu inayotupa upinzani mkubwa uwanjani iwe nyumbani au ugenini.

Haijawahi kuwa mechi rahisi kila tulipokutana na Kagera ndio maana kwenye mchezo wa leo tumechukua tahadhari zote kwakuwa malengo yetu ni kuhakikisha tunapata alama tatu.

Matola akiri ugumu wa Kagera

Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema tunategemea kukutana upinzani mkubwa kutoka kwa Kagera kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma lakini tupo tayari kuwakabili ili kufanikisha malengo tuliyojiwekea.

“Ni kweli Kagera wameshuka daraja lakini tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwao kwakuwa malengo yetu ni kuhakikisha tunapata alama zote tatu,” amesema Matola.

Mabadiliko ya kikosi (Rotation)

Kocha Msaidizi Seleman Matola ameweka wazi kuwa kutokana na ugumu wa ratiba ambao unatufanya kucheza kila baada ya siku mbili tunategemea kufanya mabadiliko ya kikosi (rotation) ili kuwapumzisha baadhi ya wachezaji.

Matola ameongeza kuwa wachezaji ni binadamu na kuwachezesha kila baada ya siku mbili kunawaathiri kiafya ndio maana huwa tunawabadilisha ili kuwapa muda wa kupumzika.

Wachezaji wapo tayari….

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinda mlango, Ally Salim amesema wapo tayari kuhakikisha tunapambana hadi mwisho ili kupata alama tatu.

Ally ameongeza kuwa tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Kagera kutokana nakuwa wana wachezaji bora ingawa tayari wameshuka daraja.

“Haitakuwa mechi nyepesi, Kagera ni timu imara na ina wachezaji wazoefu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda na kuchukua pointi tatu muhimu,” amesema Ally.

Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, Disemba 21, 2024 tuliibuka na ushindi wa mabao 5-2.

Mabao yetu yalifungwa na Shomari Kapombe, Jean Charles Ahoua, Fabrice Ngoma na Steven Mukwala aliyefunga mawili.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER