Tupo tayari kuwakabili Kengold Ali Hassan Mwinyi

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora kuikabili Kengold katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Ni mchezo muhimu kwetu ambao tunahitaji kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda taji la ligi msimu huu.

Kengold tayari wameshuka daraja lakini hiyo haifanyi tuwadharau kwakuwa alama tatu kwenye mchezo wa leo ndio kipaumbele chetu cha kwanza.

Hiki ndicho alichosema Kocha Matola…..

Kocha Msaidizi, Seleman Matola ameweka wazi malengo yetu ni kutwaa ubingwa na ili kufanikisha hilo tunahitaji kushinda mechi zetu zote tatu zilizobaki tukianza leo dhidi ya Kengold.

Matola ameongeza kuwa tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Kengold na tumejiandaa kuhakikisha tunapata alama zote tatu.

“Sisi tuna malengo ya kutwaa ubingwa msimu huu, na ili kufanikisha hilo tunahitaji kushinda mechi zote tatu zilizobaki. Tunajua Kengold wameshuka daraja lakini tunafahamu watatupa upinzani mkubwa ingawa tumejipanga kuwakabili,” amesema Matola.

Wachezaji wapo tayari kwa mchezo…..

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo mshambuliaji, Awesu Awesu amesema wapo kamili kuhakikisha malengo ya alama tatu ugenini yanafikiwa.

“Kila mchezaji anafahamu mchezo utakuwa mgumu na malengo yetu ni kupata pointi tatu kwahiyo yoyote atakayepata nafasi atakuwa tayari kupambana muda wote ili kupata ushindi ugenini,” amesema Awesu.

Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza……

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa KMC Complex, Disemba 18 tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Katika mchezo huo mabao yote yalifungwa na mshambuliaji Leonel Ateba moja likiwa kwa mkwaju wa penati.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER