Taasisi ya Super Brand imeitangaza klabu yetu ya kuwa Brand bora namba moja ya michezo nchini katika kipindi cha mwaka 2024-26.
Simba tumekuwa vinara nchini kwa upande wa Taasisi za michezo lakini tumeshika nafasi ya pili kwa ujumla miongoni mwa Taasisi 10 bora zilizopewa hadhi ya Super Brand.
Kwa mujibu wa tafiti iliyofanywa na Taasisi hiyo baada ya kuulizwa wananchi 1000 katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha wote wamekiri kuwa Simba ni Brand Bora kwa sasa nchini.
Super Brand wamekuwa wakifanya tafiti hizo kila mwaka kwa Taasisi mbalimbali nchini ikiwa na lengo la kuhamasisha ufanyaji kazi kwa ufanisi ili kuleta matokeo chanya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Doreen Bangapi amesema lengo la kutambua Taasisi hizo ni kuongeza chachu katika kutimiza majukumu kwa ufanisi mkubwa na thamani yao kutambuliwa nchini.
“Leo tupo hapa kwa ajili ya kutaja Taasisi 10 bora ambazo zimepewa hadhi yakuwa Super Brand kutokana na utendaji wake katika kipindi cha mwaka 2024-25,” amesema Bi. Doreen.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo imefanyika Hyatt Regency Hotel jijini Dar es Salaam ambapo kwa upande wa klabu yetu imepokelewa na Meneja Uendeshaji, Bi. Belinda Paul.