Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Amaan Zanzibar tayari kuikabili RS Berkane kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza ulifanyika nchini Morocco wiki iliyopita lakini bado tuna nafasi ya kupindua meza katika ardhi ya nyumbani.
Tunaiheshimu Berkane kutokana na ubora wao na uzoefu kwenye michuano hii lakini wanapaswa kujua tupo nyumbani na tupo tayari kuwakabili.
Amaan Zanzibar sio salama kwao
Baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungiwa wapinzani wetu RS Berkane walifurahia taarifa hii wakidhani itakuwa ni nafuu kwao lakini wanasahau kuwa ubora wa Simba haupo kwenye uwanja bali ni uimara wa kikosi.
Kutokana na aina ya kikosi tulichonacho tunaweza kupata ushindi kwenye uwanja wowote. Msimu huu katika michuano hii tumeshinda Angola, Libya na Tunisia na vivo hivyo tutashinda katika Uwanja wa Amaan leo.
Kauli ya Kocha Fadlu kuelekea mchezo huo
Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na kikosi chetu kipo kwenye hali nzuri kwa ajili ya kupambana.
Fadlu amesema wapinzani wetu Berkane ni timu imara na ina uzoefu wa kucheza fainali lakini tumepata muda wa kujiandaa na tupo tayari kwa ajili ya kupambana na lengo ni kuchukua ubingwa.
Sote tunafahamu kuwa Berkane ni timu nzuri na ina uzoefu kwenye michuano hii lakini tumejipanga na tupo tayari kwa ajili ya fainali na tunahitaji kushinda taji tukiwa kwenye ardhi ya nyumbani,” amesema Fadlu.
Kapombe afunguka kwa niaba ya Wachezaji
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amesema tupo tayari kwa ajili ya kupambana hadi mwisho kuhakikisha tunapata ubingwa.
Kapombe amesema tunafahamu tuna kazi kubwa ya kufanya ili kupindua matokeo ingawa haitakuwa rahisi ila tupo nyumbani na tutafanya kila linalowezekana ili kuwapa furaha Wanasimba wote.
“Kila mchezaji anafahamu umuhimu wa mchezo huu na tupo tayari kuwapa furaha Wanasimba kwa kutwaa ubingwa,” amesema Kapombe.
Rais Mwinyi aahidi donge nono
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kutoa Dola laki moja kwa wachezaji endapo tutafanikiwa kutwaa ubingwa leo.
Dkt. Mwinyi amesema kwa sasa sio suala la klabu tena bali ni la nchi nzima kama ambayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano inavyosaidia katika kila hatua na SMZ nayo haijabaki nyuma ili malengo yaliyowekwa tunatimiza.
Mwaka 1993 tulishindwa, 2025 tunabeba
Mwaka 1993 tukiwa katika ardhi ya nyumbani mbele ya Hayati Rais Ali Hassan Mwinyi tulishindwa kutwaa ubingwa wa Afrika dhidi ya Stella Club ya Ivory Coast.
Leo baada ya kupita miaka 32 tuko nyumbani tena tukiwa na mtoto wa Hayati Ali Hassan Mwinyi ambaye ni Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi.