Mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL) kati ya Simba Queens na Mashujaa Queens uliopigwa Uwanja wa KMC Complex umemalizika kwa sare ya kufungana mabao 2-2.
Mchezo huo ambao wengi walidhani ungekuwa mwepesi kutokana na wapinzani watu walivyo umekuwa tofauti na Mashujaa wamekuwa bora na walitupa ushindani mkubwa.
Asha Djafar alitupatia bao la kwanza dakika ya 38 baada ya kupokea pasi safi ya kutengwa kutoka kwa Jentrix Shikangwa kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Aisha Mnuka.
Mashujaa walipata mabao mawili na kuongoza kwa muda mrefu wa kipindi cha pili ambayo yote yalifungwa na Patricia Salum.
Jentrix alitupatia bao la kusawazisha kwa kichwa dakika ya 90 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na mlinzi wa kushoto Dotto Evarist.
Kocha wa Simba Queens Yussif Basigi alifanya mabadiliko ya kuwatoa Fatuma Issa, Elizabeth Wambui na Precious Christopher na kuwaingiza Emiliana Mdimu, Ritticia Nabbosa na Asha Rashid.
Matokeo hayo yanaifanya Queens kufikisha pointi 41 ikiendelea kubaki kileleni mwa msimamo alama tatu juu ya JKT Queens walio nafasi ya pili.