Leo ndiyo siku ambayo Tanzania na nchi jirani zitasimama kwa muda wa dakika 90 kufuatilia mchezo mkubwa wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya watani wa jadi Simba dhidi ya Yanga utakaopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mechi ya Simba na Yanga ni moja ya Derby yenye mvuto na inayofuatiliwa na watu wengi na pia ni miongoni mwa tano bora barani Afrika.
Kuelekea mchezo wa leo maandalizi yamekamilika wachezaji wote wako tayari na hakuna atakayekosekana kwa sababu yoyote.
Kocha msaidizi, Seleman Matola ameweka wazi kuwa mchezo utakuwa mgumu na haijawahi kutokea mechi ya Derby ikawa rahisi lakini tumejiandaa kushinda.
Matola amesema licha ya kufahamu mchezo utakuwa mgumu lakini tumejiandaa kucheza soka safi la burudani kama ilivyo kawaida yetu.
“Tunajua mchezo utakuwa mgumu hii ni Derby na haijawahi kuwa rahisi lakini tumejiandaa kushinda. Lengo letu ni kutetea ubingwa wa ligi na ili tufanikiwe tunapaswa kushinda kila mchezo ukiwemo wa leo,” amesema Matola.
Matokeo ya mechi tatu zilizopita tulipokutana.
Septemba 7, 2020
Yanga 1-1 Simba
Machi 8, 2020
Yanga 1-0 Simba
Januari 04, 2020
Simba 2-2 Yanga
Hadi sasa tumecheza jumla ya mechi 25 za Ligi Kuu, tukishinda michezo 19, sare nne na kufungwa miwili tukiwa na pointi 61 alama nne juu ya Yanga huku tukiwa na michezo miwili mkononi.