Kocha Msaidizi, Seleman Matola ameweka wazi kuwa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wetu kutokuwa kwenye nafasi nzuri.
Matola amesema pamoja na ubora walionao KMC lakini bado hawapo nafasi nzuri kwenye msimamo hivyo lazima wapambane kutafuta alama tatu katika uwanja wa nyumbani ingawa tupo tayari kuwakabili.
Matola ameongeza kuwa ratiba yetu ni ngumu kutokana na kucheza mechi kila baada ya siku mbili ndio maana tumekuwa tukifanya mabadiliko ya kikosi mara kwa mara.
“Nikiri tu tuna ratiba ngumu, hatupati muda mwingi wa maandalizi lakini tuna kikosi kipana ambacho kinaweza kutuwezesha kupata ushindi popote. Tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa KMC lakini tumejipanga kupata matokeo chanya,” amesema Matola.
Akiongea kwa niaba ya wachezaji mlinda mlango, Hussein Abel amesema pamoja na ugumu ambao tunatarajia kukutananao lakini tumejipanga kupambana hadi mwisho kupata pointi tatu.
“Mchezo utakuwa mgumu KMC ni timu imara yenye wachezaji wazuri, tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini Simba ni kubwa na tutaingia kwa malengo ya kupata pointi tatu,” amesema Abel.