Muda mfupi baada ya kutangazwa Kocha Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania, Kocha Mkuu Didier Gomez amesema tuzo hiyo ni kwa ajili ya benchi zima la ufundi si yake peke yake.
Gomez amesema siku zote wanafanya kazi kama timu na kila mmoja anatimiza majukumu yake ipasavyo ndiyo ameamua kuigawa kwa benchi nzima la ufundi.
Gomez raia wa Ufaransa ameongeza kuwa kushinda tuzo binafsi ni jambo zuri na linaongeza morali ya kazi lakini anafurahi zaidi ushirikiano anaoupata kutoka kwa wasaidizi wake.
“Nafurahishwa na wasaidizi wangu, kocha msaidizi, kocha wa viungo, kocha wa makipa na meneja, wanafanya kazi nzuri na hii ni tuzo yetu sote,” amesema Kocha Gomez.
Hii ni tuzo ya kwanza ya kocha bora wa mwezi wa ligi kwa Gomez tangu alipojiunga nasi Februari mwaka huu.