Tumeingia Mkataba na Jayrutty kwa ajili ya utengenezaji wa vifaa vya Michezo

Klabu yetu imeingia mkataba wa miaka mitano na Kampuni ya Jayrutty Investment Company East African Limited kwa ajili ya kutengeneza, kubuni na kusambaza vifaa vya michezo wenye thamani ya Shilingi bilioni 38.

Mwenyekiti wa Kamati ya Tenda, Dkt. Seif Muba amesema walifanya mchakato wa wazi kwa wote waliomba tenda hiyo na aliyokidhi matakwa ambayo itakuwa na faida kubwa kwa klabu ni Kampuni ya Jayrutty Investment East African Limited.

Dkt. Muba amesema kwa mujibu wa mkataba huo Kampuni ya Jayrutty itakuwa inatoa Shilingi bilioni 5.6 kwa mwaka ambapo itakuwa inaongezeka kwa asilimia 10 kila mwaka katika kipindi chote cha miaka mitano.

“Nipo mbele yenu kumtangaza mshindi wa zabuni ya kutengeneza, kubuni na kusambaza vifaa vya michezo ya Jayrutty Investment katika kipindi cha miaka mitano. Tumefanya mchakato huu kwa uwazi na pande zote zilishirikishwa kwenye kila hatua mpaka tenda ilipokamilika na kusaini mkataba,” amesema Dkt. Muba.

Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Jayrutty Investment, CPA. Joseph Rwegasira amesema mbali na kiasi hicho cha pesa cha Shilingi bilioni 38 kwenye kipindi cha miaka mitano kuna faida mbalimbali ambazo Klabu yetu itaipata.

CPA. Rwegasira ametaja faida hizo kuwa ni kujenga Uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 10,000 mpaka 12,000, Kununua basi la kisasa la Irizar, Kujenga Ofisi za kudumu za Klabu, Kutengeneza Studio ya kisasa kwa ajili ya kurusha maudhui ya Habari.

Faida nyingine alizotaja CPA. Rwegasira ni kutoa kiasi cha milioni 100 kwa ajili ya kukuza soka la vijana, kutoa milioni 100 kwa maandalizi ya msimu (Pre Season), na pia watatoa kiasi cha milioni 470 kwa ajili ya kuongeza motisha kwa wachezaji na hiyo itakuwa kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano.

“Tunaushukuru Uongozi wa klabu ya Simba kwa kutupa dhamana hii, nami nipo hapa kuwahakikishia Wanasimba wote kuwa kuanzia msimu ujao tutakuwa na jezi bora za Kimataifa na Klabu yetu itakuwa ya kwanza katika historia ya nchi,” amesema CPA Rwegasira.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER