Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema Uongozi unafanya mawasiliano na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ili aweze kuwa mgeni Maalum katika mchezo wetu wa marudiano wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry utakaopigwa Jumatano ijayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Ahmed ameyasema wakati wa ufunguzi wa hamasa kuelekea mchezo huo ambazo zimefanyika Mbezi Shule Sokoni zikiwa na lengo la kuwataka mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa sapoti timu ili kuweza kupata nafasi ya kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo.
Ahmed ameongeza kuwa sababu ya kumualika Rais Karia ni kumpa heshima na kuthamini mchango wake katika kuleta maendeleo ya soka nchini pamoja na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
“Tunategemea Rais wa TFF Wallace Karia atakuwa mgeni Maalum kwenye mchezo wetu wa marudiano dhidi ya Al Masry. Ametenda mengi kwenye mpira Tanzania na mafanikio tuliyonayo Simba Kimataifa yametokana na uimara wake.
“Simba tunatambua, tunathamini na kuheshimu mchango wa Rais Karia, leo kufikia nafasi ya sita kwenye viwango vya ubora Afrika ni kutokana na uongozi wake thabiti hivyo hatuna budi kumpa heshima hii ya kipekee na kumualika kuwa mgeni maalum wa mchezo wetu dhidi ya Al Masry siku ya Jumatano,” amesema Ahmed.