Timu yarejea mazoezini kujiandaa na Tabora United
Kikosi chetu kimerejea mazoezini jana kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tabora United utakaopigwa Jumapili, Februari 2 katika Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema wachezaji wote waliokuwa wamepewa mapumziko tayari wamerejea na kikosi kamili kimeanza mazoezi.
Ahmed amesema wachezaji wataendelea na mazoezi kwa siku tatu ambapo Jumamosi kikosi kitaanza safari ya kuelekea Tabora tayari kwa mchezo huo.
“Wachezaji walipewa mapumziko ya siku chache baada ya ushindi wa mabao 6-0 tuliopata dhidi ya Kilimanjaro Wonders wikiendi iliyopita.
“Kuna wale ambao walipewa mapumziko marefu kidogo hasa wa kikosi cha kwanza nao wamerejea na wanaendelea na mazoezi. Tunafahamu itakuwa mechi ngumu lakini tunaendelea na maandalizi lengo ni kuchukua alama zote tatu,” amesema Ahmed.
Mchezo dhidi ya Tabora utakuwa ni wa kwanza katika mzunguko wa pili wa ligi ambayo tutaingia tukiwa kileleni mwa msimamo.