Kikosi chetu leo kimefanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kabla ya kuanza safari ya kuelekea Shinyanga kuikabili Mwadui FC.
Mchezo huo wa Ligi Kuu utapigwa katika dimba la Kambarage kesho Jumapili saa 10 jioni.
Wachezaji wote 28 waliosafiri na timu wamefanya mazoezi na wako katika hali nzuri hivyo Kocha Didier Gomez na wasaidizi wake watakuwa na wigo mpana kupanga kikosi kulingana na mahitaji ya mchezo.
Kikosi kiliwasili jijini hapa jana usiku kwa hiyo wamefanya mazoezi ya kuweka miili sawa kutokana na uchovu wa safari ya kutoka jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa kesho utakuwa ni wa kwanza wa mkoani tangu timu ilipomaliza mechi za hatua ya makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika na kufanikiwa kumaliza vinara wa kundi A.
Kikosi kitaondoka jijini hapa muda mfupi ujao kuelekea Shinyanga kwa basi tayari kwa mchezo wa kesho.