Tupo kwa Mkapa kumalizia kazi tuliyoianza

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili CS Constantine kutoka Algeria katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Utakuwa mchezo mgumu ambao utaamua nani atakuwa kinara wa kundi baina yetu na Constantine.

Pamoja nakuwa tumefuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini leo tunahitaji kushinda ili kuwa vinara wa kundi.

Fadlu amesema hatuna presha…..

Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema pamoja na ukubwa na umuhimu wa mchezo wenyewe ambao kila timu inahitaji alama tatu lakini hatutacheza kwa presha.

Fadlu amesema tutacheza soka letu tulilolizoea lakini kwa kuchukua tahadhari zote kwakuwa jambo muhimu ni kuhakikisha tunapata alama zote tatu.

“Haiwezi kuwa mechi rahisi kwakuwa tunahitaji kushinda ili kuongoza kundi na wenzetu wanahitaji hata alama moja lakini hatuna presha tutacheza soka letu tulilolizoea.” amesema Fadlu.

Wachezaji wanaitaka mechi…….

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo mshambuliaji, Awesu Awesu amesema wapo tayari kuhakikisha tunapata ushindi na kuongoza kundi ili kuwaburudisha Wanasimba.

Awesu amezungumzia pia kuhusu kukosekana kwa mashabiki kuwa wachezaji wameumia lakini kupitia dua na maombi mbalimbali wanaamini wataweza kushinda na kupata pointi tatu na kuongoza kundi.

“Sisi tupo tayari na tunajua kwetu ni kama fainali kwakuwa tunahitaji ushindi ili kuongoza kundi na uwezo huo tunao. Tunahitaji sala na maombi kutoka kwa mashabiki wetu,” amesema Awesu.

Sababu za kupambana kupata ushindi hizi hapa:

Tunahitaji alama tatu ili kuongoza kundi (Kuweka heshima).

CS Constantine ndio timu pekee ambayo hatujaifunga kwenye hatua ya makundi na pia ilitufunga kwao (tunataka kulipa kisasi).

Tunataka kuendeleza ‘umwamba’ na kulinda heshima katika uwanja wa nyumbani (Kwa Mkapa hatoki mtu).

Tunataka kuwapa furaha Wanasimba kushuhudia timu ikimaliza hatua ya makundi kwa kishindo.

Tunaweka rekodi mpya….

Kwa mara ya kwanza mchezo wetu katika michuano ya Afrika hautakuwa na mashabiki.

Haijawahi kutokea huko nyuma lakini kutokana na adhabu tuliyopata kutoka CAF itatulazimu kucheza mechi ya muhimu nyumbani bila uwepo wa mashabiki.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER