Uongozi wa klabu ukishirikiana na Mo Dewji Foundation umetoa zawadi mbalimbali katika Kituo chenye uhitaji cha Sinza ikiwa sadaka kuelekea mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine utakaopigwa Jumapili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Huu ni utaratibu tuliyojiwekea wa kutoa misaada mbalimbali kwa jamii yenye uhitaji kwakuwa tunaamini hakuna jambo lolote ambalo tunaweza kulifanya bila kibali cha Mwenyezi Mungu.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema tunahitaji kupata ushindi kwenye mchezo wa Jumapili ndio maana tumerejea kwa Mungu na kupitia sadaka tuliyotoa kwa Kituo cha Sinza itakuwa ni sehemu ya kufanikiwa katika malengo yetu.
“Kama mnavyofahamu Jumapili tunacheza dhidi ya Constantine na tunahitaji kupata ushindi na ndio sababu ya kujikurubisha nakupitia dua na sadaka tuliyotoa wachezaji watakuwa timamu kwa ajili ya kuhakikisha timu inapata ushindi,” amesema Ahmed.
Kwa upande wake Msimamizi wa Kituo cha Kiislamu cha Sinza ambaye pia ni Imamu wa Msikitini wa Rahman, Sheikh Ally Abdallah ameushukuru Uongozi kwa kushirikiana na Mo Dewji Foundation kwa misaada hiyo huku akisema kupitia sadaka hiyo Mwenyezi Mungu atatusaidia kufikia malengo yetu.
Nae Ofisa Mahusiano na Maji kutoka Mo Dewji Foundation, Steve Salum amesema mara zote lengo lao ni kuhakikisha wanaigusa jamii katika nyanja mbalimbali ndio mara zote wamekuwa wakishirikiana na Uongozi wa Klabu.
“Kusaidia watu wenye uhitaji ni moja ya lengo kuu la Mo Dewji Foundation ndio maana tupo hapa, tunaamini kwa sadaka hii itasaidia timu yetu ya Simba kupata ushindi kwenye mchezo wa Jumapili,” amesema Steve.