Menejimeti ya Klabu imepokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau na Wanachama kuhusu faini iliyotolewa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) ya kufungiwa kuingiza mashabiki kwenye mchezo wetu dhidi ya CS Constantine pamoja na faini ya dola milioni 40 sawa na takribani milioni 100 kutokana na vurugu zilizotokea kwenye mechi yetu dhidi ya CS Sfaxien, Disemba 15.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema kilichotokea ni kosa kwa Wanasimba wote na hakuna haja ya kunyoosheana vidole ambapo baada ya mjadala mrefu, Viongozi wa Klabu tumekuja na kampeni ya ‘Tunawajabika Pamoja’ ambayo tutachangia kupitia mitandao ya simu ya Vodacom, Airtel Money na Mixx By Yas ili kulipa faini hiyo.
Ahmed amesema Kampeni hii itaonyesha uwajibikaji wa kila Mwanasimba kutokana na kilichotokea kwakuwa kila mmoja ataweza kuchangia alichonacho ili kufanikisha kulipa faini hii.
“Kila mtu anafahamu kilichotokea na hatuna haja ya kurudia, jana tumepokea hukumu kutoka CAF ya kufungiwa kuingiza mashabiki pamoja na faini ya dola milioni 40 na kupitia maoni ya mashabiki tumekuja na kampeni ya ‘Tunawajibika Pamoja’ ili kuchangia kulipa faini hii.
“Kuanzia sasa kila Mwanasimba ataweza kuchangia kiasi alichonacho kupitia namba zetu za Lipa kwa simu katika mitandao ya Vodacom, Airtel Money na Mixx By Yas na tumezitoa namba kwenye mitandao yetu yote ya kijamii,” amesema Ahmed.
Namba za kutuma pesa ni kama zifuatazo:
Mixx By Yas Jina SIMBA SC namba 6179540
Airtel Money Jina SIMBA SC namba 954545
Vodacom Jina SIMBA SC Namba 5306272
Aidha Ahmed ameongeza kuwa hakuna Mwanasimba mwenye Mamlaka ya kuchangisha kwenye magroup wala Matawi badala yake kila mmoja atume kwenye namba tajwa hapo ili kuondoa sintofahamu.
Zoezi la kuchangia limeanza sasa na litamalizika Jumapili baada ya kuanza mchezo dhidi ya Constantine na tutakuwa tunatoa mrejesho kila baada ya muda kwenye mitandao yetu kama tunavyofanya kwenye mauzo ya tiketi.