Tupo tayari kuikabili Bravos Novemba 11 Leo

Saa moja usiku wa leo kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Novemba 11 nchini Angola kuikabili Bravos Do Marquis katika mchezo wa tano wa kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Ni mchezo mgumu na muhimu ambao matokeo yake yatakuwa yanaamua nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali kwa timu zote.

Ni mechi ya mtego hivyo tutaingia uwanjani kwa umakini mkubwa kwani tukishinda au kutoka sare tutakuwa tumejihakikishia kufuzu moja kwa moja huku Bravos nao wakipata alama tatu leo watafikisha tisa ambazo zitawarejeshea nafasi ya kufuzu baada ya mechi ya mwisho.

Fadlu anajua jinsi Bravos wanavyocheza nyumbani

Kocha Mkuu Fadlu Davids ameweka wazi moja ya mbinu wanayotumia Bravos kucheza hasa mechi za nyumbani ni kutumia nguvu nyingi ili kuwachanganya wapinzani.

Fadlu amesema kwa kuliona hilo amekiandaa kikosi chetu kucheza soka la kumiliki mpira muda mrefu ikiwa ni mipango ya kuwadhibiti na kufanya mashambulizi ya haraka yatakayotupatia matokeo chanya.

“Tunaifamu vizuri Bravos ikicheza nyumbani inacheza vingine na nje ya nyumbani inacheza vingine, wapo vizuri kwenye kuanzisha mashambulizi baada ya kupora mpira kwahiyo tunatakiwa kumiliki zaidi mchezo,” amesema Kocha Fadlu.

Debora afurahia kurudi nyumbani….

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo, Debora Fernandes ambaye amecheza nchini Angola kwa miaka miwili amesema utakuwa mchezo mgumu kutokana na Bravos kuhitaji alama tatu ili kufufua matumaini ya kufuzu robo fainali lakini malengo yetu ni kuhakikisha tunapata matokeo chanya.

“Nimefurahi kurudi nyumbani nimecheza Angola kwa miaka miwili, nimewaambia wachezaji wenzangu mambo mbalimbali kuhusu hapa ili wajue mazingira na aina ya mchezo utakaochezwa,” amesema Debora.

Tuna kumbukumbu nzuri Novemba 11

Mara ya mwisho kucheza katika Uwanja wa Novemba 11 ilikuwa Oktoba 9, 2022 dhidi ya Primiera De Agosto katika mchezo hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na tulifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Katika mchezo huo mabao yetu yalifungwa na Clatous Chama, Israel Patrick na Moses Phiri.

Watano walikuwepo kwenye mchezo dhidi ya De Agosto

Katika kikosi cha Wachezaji 22 walipo Angola ni nyota watano pekee ambao walikuwepo tulivyokuja mara ya mwisho katika Uwanja wa Novemba 11 tulipoifunga De Agosto 3-1.

Nyota hao ni Ally Salim, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Zimbwe, Mzamiru Yassin na Kibu Denis.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER