Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema kikosi chetu kipo tayari kwa ajili ya mchezo watano wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos Do Marquis utakaopigwa Jumapili Januari 12 katika Uwanja wa Novemba 11 nchini Angola.
Kocha Fadlu amesema anaamini utakuwa mchezo mgumu hasa kutokana na jinsi kundi letu lilivyo lakini tumejiandaa vizuri huku akisema hali ya hewa sio changamoto kwakuwa ni sawa na nyumbani.
Fadlu ameongeza kuwa Bravos ni tofauti inapocheza nyumbani hivyo amejipanga kuhakikisha wachezaji wetu Wana miliki mchezo muda mwingi ikiwa ni sehemu ya kutufanya kuwa salama dhidi yao.
“Tunaifahamu vizuri Bravos ikicheza nyumbani inacheza vingine na nje ya nyumbani inacheza vingine, wapo vizuri kwenye kuanzisha mashambulizi baada ya kupora mpira kwahiyo tunatakiwa kumiliki zaidi mchezo,” amesema Kocha Fadlu.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo, Debora Fernandes ambaye amecheza nchini Angola kwa miaka miwili amesema utakuwa mchezo mgumu kutokana na Bravos kuhitaji alama tatu ili kufufua matumaini ya kufuzu robo fainali lakini malengo yetu ni kuhakikisha tunapata matokeo chanya.
Debora ameongeza kuwa kikosi chetu kinaundwa na wachezaji wengi wapya ambao wapo tayari kujitoa kwa ajili ya kuisaidia timu kufikia malengo na hilo ndilo jambo jema kwa sasa.
“Utakuwa mchezo mgumu natambua Bravo wanacheza nyumbani na wanahitaji pointi tatu ila anajua malengo ya Simba ni kuhakikisha tunafanya vizuri.”
“Nimefurahi kurudi nyumbani nimecheza Angola kwa miaka miwili, nimewaambia wachezaji wenzangu mambo mbalimbali kuhusu hapa ili wajue mazingira na aina ya mchezo utakaochezwa,” amesema Debora.