Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema tunahitaji kucheza soka safi pamoja na kuhakikisha tunapata pointi tatu kwenye mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi Ken Gold utakaopigwa Uwanja wa KMC Complex saa 10 jioni.
Kocha Fadlu amesema baada ya kumaliza vema mechi zetu za Kombe la Shirikisho Afrika sasa ni muda wa kuhamishia nguvu kwenye ligi na mchezo wa kesho tunahitaji kufanya vizuri.
Fadlu ameongeza kuwa ratiba ya ligi imebana kutokana na kutakiwa kucheza mechi nne ndani ya muda mfupi hivyo ni bora kuhakikisha unafanya vizuri kwenye kila mechi.
Akizungumzia kuhusu hali ya kikosi kocha Fadlu amesema ataangalia baada ya mazoezi ya leo jioni kuona ni wachezaji gani watakuwa tayari kwa ajili ya mchezo kwakuwa kuna baadhi walipata maumivu kwenye mechi zilizopita.
“Nimepata muda wa kutazama baadhi ya mechi za Ken Gold ukiwemo dhidi ya Namungo ni timu nzuri lakini tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye Uwanja wa nyumbani,” amesema Kocha Fadlu.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo mshambuliaji, Awesu Awesu amesema kwa upande wao wapo tayari kuhakikisha ushindi unapatikana kwenye mchezo wa kesho.
“Kila mchezo ambao Simba inacheza ni kama fainali na kesho tunajua itakuwa mechi ngumu lakini wachezaji tupo tayari kupambana kuhakikisha ushindi unapatikana,” amesema Awesu.