Leo saa moja usiku kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Chahid Hamlaoui kuikabili CS Constantine kutoka Algeria katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ni mechi ya pili ya hatua ya makundi pia ni mchezo wa kwanza ugenini hivyo tunaamini utakuwa mchezo mgumu na tumejipanga kwa hilo.
Tunahitaji kushinda na kuonyesha soka safi katika mchezo wa leo ili kukaa kileleni mwa msimamo.
Maneno ya Kocha Fadlu Davids….
Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema tumepata siku tatu za kufanya mazoezi nchini Algeria na wachezaji wamezoea hali ya hewa ya baridi kali na maandalizi yamekamilika.
Kocha Fadlu ameongeza kuwa itakuwa ni jambo jema kwetu kupata ushindi na ikishindikana basi tupate sare alama moja ugenini bado ni matokeo mazuri.
“Kikosi chetu kipo kwenye hali nzuri kwa ajili ya mchezo wa leo, jana tumefanya mazoezi ya mwisho na wachezaji wapo kweli hali nzuri tayari kwa mechi ambayo tunaamini itakuwa ngumu lakini tumejipanga kupata matokeo chanya,” amesema Kocha Fadlu Davids.
Wachezaji wanaitaka mechi……
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mshambuliaji, Leonel Ateba amesema kwa upande wao wapo tayari na kila atakayepata nafasi amejipanga kufanya vizuri ili kuwapa furaha Wanasimba.
“Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu hasa ukichangiwa zaidi nakuwa tupo ugenini lakini tumejiandaa kupambana mpaka mwisho kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema Leonel Ateba.
Hatujawahi kukutana na CS Constantine…
Licha ya kuja mara kadhaa nchini Algeria kucheza mechi kwenye michuano hii lakini tulikuwa hatujawahi kukutana na CS Constantine na leo ni mara ya kwanza.
CS Constantine ni timu bora kwa sasa nchini Algeria na inafanya vizuri pia kwenye ligi ya Algeria lakini kwa uzoefu tulionao kwenye michuano hii tuna matumaini makubwa ya kufanya vizuri Leo.
Ni fainali ya Kundi….
Mchezo wa leo ni kama fainali kwenye kundi kwakuwa timu zote zimeshinda mchezo wa kwanza kwa bao moja hivyo mshindi atahakikisha kuwa kinara wa kundi.