Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Bravos Do Marquis kutoka Angola katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.
Mbali nakuwa ni mechi ya kwanza ya hatua ya makundi pia ni mchezo wa kwanza wa nyumbani hivyo ni muhimu kwetu kuhakikisha tunashinda.
Tunahitaji kushinda na kuonyesha soka safi katika mchezo wa leo ili kuwafurahisha mashabiki ambao tunaamini watakuja kwa wingi.
Maneno ya Kocha Fadlu Davids….
Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema tumepata siku nne za kufanya mazoezi tangu tulivyocheza mechi ya ligi ya mwisho dhidi ya Pamba Jiji na wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri.
Kocha Fadlu ameongeza kuwa itakuwa ni jambo jema kwetu kuanza kwa ushindi hasa tukiwa nyumbani ingawa haitakuwa kazi rahisi lakini tumejipanga na tupo tayari.
“Ni mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho ambao tunacheza katika Uwanja wa nyumbani ni muhimu kwetu kupata ushindi na kuwafurahisha mashabiki ambao tunaamini watakuja kwa wingi kutupa sapoti,” amesema Kocha Fadlu.
Wachezaji wanaitaka mechi……
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kati, Che Fondoh Malone amesema kwa upande wao wapo tayari na kila atayepata nafasi amejipanga kufanya vizuri.
“Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu lakini tupo nyumbani na tuna faida yakucheza mbele ya mashabiki wetu na tumejiandaa kuwapa furaha,” amesema Che Malone.
Mashabiki waitwa kwa Mkapa……….
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani leo ili kuwasapoti wachezaji kwakuwa kinachohitajika ni alama tatu.
“Ushindi kwenye mchezo wa leo hautatokana na Viongozi, benchi la ufundi wala wachezaji pekee bali ni wingi wa mashabiki uwanjani ambao utaongeza hamasa kwa nyota wetu itakayotuletea furaha kwa kuifunga Bravos,” amesema Ahmed.