Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa KMC Complex kuikabili Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo wa leo utakuwa ni watano wa ligi ambapo mechi nne tulizocheza tumeshinda zote na hatujaruhusu bao.
Tutaingia kwenye mchezo huu tukiwa na morali kubwa huku tukiwa na umuhimu mkubwa wa kupata pointi tatu ambazo zitatufanya kukaa kileleni mwa msimamo.
Hiki ndicho Alichosema Fadlu……..
Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema mchezo utakuwa mgumu hasa baada ya Coastal kubadilika kiuchezaji lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.
Kocha Fadlu amesema tutahakikisha tunatumia vizuri kila nafasi itakayopatikana kufunga huku tukichukua tahadhari zote kwenye ulinzi.
“Ratiba ni ngumu tumecheza mechi tatu ndani ya wiki, tunatengeneza uwiano wa wachezaji kwakuwa kuelekea Disemba mechi zitazidi kuwa karibu karibu kwahiyo kila mchezaji anatakiwa kuwa timamu.
“Malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo, hauwezi kuwa bingwa kwa kushinda mechi nne, tunatakiwa kuendelea kukusanya pointi na kuhakikisha tunaweza pia kuzuia vizuri,” amesema Kocha Fadlu.
Wachezaji wapo tayari……..
Kwa upande wake nahodha wa timu, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema kwa upande wao wachezaji wapo tayari kufuata maelekezo watayopewa ili kuisaidia timu kupata ushindi.
“Sisi wachezaji tupo tayari, tunaiheshimu Coastal kutokana na ubora wao ila lengo letu ni kuhakikisha tunashinda tukiwa nyumbani na kuwapa furaha mashabiki wetu,” amesema Zimbwe Jr.
Mara ya mwisho tuliwafunga…..
Katika mchezo wa mwisho tuliokutana na Coastal Union Machi 9 mwaka huu katika Uwanja CCM Mkwakwani tuliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Kwenye mchezo huo mabao yetu yalifungwa na Freddy Michael Kouablan na Willy Onana huku lile la Coastal likifungwa na Lucas Kikoti.
Mzamiru na Kagoma warejea…….
Viungo wetu wakabaji Mzamiru Yassin na Yusuph Kagoma wamerejea kikosini na mwlimu Fadlu Davids anaweza kuwatumia kama ataona inafaa baada ya kupona majeraha.