Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Al Ahli Tripoli katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bila kufungana wiki iliyopita nchini Libya.
Hakuna jambo lolote linalohitajika zaidi ya ushindi kwenye mchezo wa leo ili kuiwezesha timu kutinga hatua ya makundi.
Kocha Fadlu atoa kauli…….
Kocha Fadlu amesema tutacheza kwa umakini mkubwa hasa katika safu ya ulinzi kwani hatupaswi kuruhusu bao huku pia tukitakiwa kuhakikisha tunapata mabao zaidi.
Kocha Fadlu ameongeza kuwa itakuwa mechi ngumu lakini tutakuwa na faida kwakuwa tupo nyumbani na mashabiki wetu watakuwa nyuma yetu.
“Tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho, itakuwa mechi ngumu kwakuwa inahusisha timu mbili kubwa ambazo sio tu zinawaza kuingia hatua ya makundi bali kuchukua ubingwa wenyewe,” amesema Kocha Fadlu.
Zimbwe Jr afunguka…….
Nahodha wa timu Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema kwa upande wa wachezaji wapo tayari kuhakikisha wanapambana ili kuiwezesha timu kuingia hatua ya makundi.
“Hali kama hii imewahi kututokea mara nyingi huko nyuma na hatuna presha tunajua Wanasimba wanahitaji furaha nasi tupo hapa kuhakikisha hilo linafanikiwa,” amesema Zimbwe Jr.
Mzamiru kuikosa Al Ahli Tripoli leo…
Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema kiungo mkabaji Mzamiru Yassin hatakuwa sehemu ya kikosi katika mchezo wa leo kutokana na kupata maumivu kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Fadlu ameongeza kuwa Mzamiru anafanya mazoezi pamoja na wenzake lakini hali yake haimuwezeshi kucheza mchezo wa leo.