Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema kikosi chetu kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli utakaopigwa saa mbili usiku.
Kocha Fadlu amesema kikosi kimepata siku mbili ya kufanya mazoezi nchini Libya ambazo zimewasaidia kuzoea hali ya hewa na wamefanya katika Uwanja tutakaocheza kesho.
Akizungumzia mchezo wenyewe Fadlu amesema utakuwa mgumu hasa kutokana na Tripoli kufanya usajili wa wachezaji wengi bora na wenye uzoefu wa michuano hii.
“Tunafahamu kesho uwanja utakuwa na mashabiki wengi ambao watakuja kuipa sapoti timu yao lakini tumewaandaa wachezaji kukabiliana na hilo,” amesema Kocha Fadlu.
Kwa upande wake nahodha wa timu, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema wachezaji wapo tayari kufuata maelekezo tutakayopewa na walimu ili kukamilisha lengo na mipango ya timu.
Zimbwe Jr amesema tunafahamu utakuwa mchezo mgumu na tunawaheshimu wapinzani wetu hasa ukizingatia tupo ugenini.
“Kwa upande wetu wachezaji tupo kwenye hali nzuri kwa ajili ya mchezo wa kesho, kila atayepata nafasi atakuwa tayari kuipigania timu kupata matokeo chanya,” amesema Zimbwe Jr.