Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema mchezo wa kesho wa kutafuta mshindi wa tatu wa Ngao ya Jamii utatuweka kwenye nafasi nzuri kuelekea mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya NBC ambayo tutacheza na Tabora United.
Kocha Fadlu amesema ni muhimu kushinda kila mechi kwakuwa Simba ni timu kubwa na inapigania mataji kila msimu.
Kocha Fadlu ameongeza kuwa itakuwa mechi ngumu kutokana na ubora wa wapinzani lakini tuna timu imara ambayo inaweza kutuwezesha kupata ushindi.
“Utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa Coastal, kufungwa mabao matano sio kwamba ni timu dhaifu, tutaingia kwa kuiheshimu, ushindi ni jambo la muhimu kwetu,” amesema Kocha Fadlu.
Akizungumzia uwezekano wa kusajili mchezaji mpya kabla ya kufungwa kwa dirisha Agosti 15, Fadlu amesema “najivunia kikosi nilichonacho lakini tukipata mchezaji sahihi tunaweza kumuongeza, ninapata msaada mkubwa kutoka kwa Uongozi wangu.”
Akizungumzia kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kati, Hussein Kazi amesema hayakuwa malengo yetu kucheza mshindi wa tatu lakini kwakuwa ndio matokeo ya mpira tuko tayari kupambana.
“Sisi kama wachezaji tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho, tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema Kazi.