Tunafunga msimu kwa kucheza na JKT Tanzania

Msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2023/24 unamalizika rasmi leo na kikosi chetu kitakuwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili JKT Tanzania.

Ni mchezo ambao tunahitaji kupata alama tatu ili kuyafanya matumaini yetu ya kumaliza nafasi mbili za juu kukamilika.

Kila mmoja anafahamu kuwa itakuwa mechi ngumu kwa sababu wapinzani wetu JKT hawapo kwenye nafasi nzuri katika msimamo hivyo watataka kupambana ili kujinasua.

Kila kitu kipo tayari….

Kaimu Kocha Mkuu Juma Mgunda amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na kikosi kipo tayari kwa ajili ya kupambana.

Mgunda amesema ni mchezo muhimu kwetu kupata pointi tatu ambazo zitatuweka kwenye mazingira mazuri ya kumaliza nafasi mbili za juu huku tukisubiri matokeo ya timu nyingine.

“Maandalizi ya mchezo yamekamilika na timu ipo kwenye hali nzuri kuhakikisha tunashinda mchezo wa mwisho ili tupige hesabu zetu tukiwa na alama tatu,” amesema Mgunda.

Kibu arejea…..

Kiungo mshambuliaji, Kibu Denis ambaye alikuwa majeruhi amerejea kikosini na jana amefanya mazoezi ya mwisho na wenzake kwa ajili ya mchezo wa leo.

Kwa mujibu wa taarifa za daktari, Kibu yupo tayari kwa ajili ya kuendelea kucheza hivyo ni juu ya benchi la ufundi kumtumia katika mchezo wa leo.

Tuliwafunga mzunguko wa kwanza…

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi uliopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo tuliibuka na ushindi wa bao moja.

Bao letu lilifungwa na kiungo mshambuliaji Clatous Chama kwa shuti kali nje ya 18 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Saido Ntibazonkiza.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER