Leo tupo Azam Complex kuikabili Tabora

Kikosi chetu leo 12:15 jioni kitashuka katika Uwanja wa Azam Complex kuikabili Tabora United katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tunaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-0 tuliopata dhidi Mtibwa Sugar siku tatu zilizopita.

Pamoja na ubora walionao Tabora lakini tumejiandaa kuhakikisha tunashinda ili kuzidi kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo.

Mgunda atoa neno…..

Kocha Mkuu Juma Mgunda amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na wachezaji wapo hali nzuri tayari kupigania pointi tatu.

Mgunda amesema tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa tunafahamu tunacheza na timu ambayo ipo kwenye ligi kama sisi bila kujalisha ipo kwenye nafasi gani.

“Tupo tayari kwa mchezo wa leo, wachezaji wapo kwenye hali nzuri. Lengo letu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo.

“Tunaenda kupambana na Tabora tukiwa tunajua haipo kwenye nafasi nzuri lakini huu ni mpira hatuwezi kuwadharau, tutaingia kwa tahadhari zote lakini tunahitaji kushinda mchezo,” amesema Mgunda.

Tuliwafunga 4-0 mzunguko wa kwanza….

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja Ali Hassan Mwinyi, Februari 6, tuliibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Kwenye mchezo huo mabao yetu yalifungwa na Pa Omar Jobe, Sadio Kanoute, Che Fondoh Malone na Freddy Michael Kouablan.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER