Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi kuikabili Mtibwa Sugar katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa tunafahamu tuna dhima kubwa kutoka kwa mashabiki wetu kutokana na matokeo tuliyopata katika mechi zetu zilizopita.
Mchezo wa leo ni muhimu kwetu kupata pointi tatu ili kurejesha hali ya kujiamini na kuendelea kushinda ili kujiweka kwenye mazingira mazuri katika msimamo.
Mgunda azungumzia hali ya timu….
Kocha Mkuu Juma Mgunda amesema pamoja na timu ya Mtibwa Sugar kutokuwa kwenye nafasi nzuri lakini hatuwezi kuwadharau badala yake tutaingia kwa tahadhari.
Mgunda amesema wakati ligi inaelekea ukingoni kila timu inajitajidi kufanya vizuri ili kujitoa kwenye nafasi mbaya na kumaliza vizuri.
“Hii ni Ligi na hakuna timu dhaifu. Mtibwa ni timu bora na tunaiheshimu na tumejiandaa kuhakikisha tunapata pointi tatu.
“Siku zote kwenye kila mchezo kunakuwa na mazuri na mabaya yale mazuri tunayaongeza na mapungufu tunayapunguza au kuyaondoa kabisa, tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Mgunda.
Mzamiru, Ntibazonkiza warejea kikosini….
Kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin ambaye aliukosa mchezo uliopita dhidi ya Namungo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano amerejea kikosini na anategemewa kuwa sehemu ya kikosi cha Leo.
Saido Ntibazonkiza ambaye alikuwa ana maumivu aliyopata kwenye michuano ya Kombe la Muungano kule Zanzibar nae amepona na jana amefanya mazoezi ya mwisho na yupo tayari kwa mchezo wa leo.
Chama afungiwa…..
Kiungo mshambuliaji Clatous Chama atakosekana kwenye mchezo wa leo kutokana na kufungiwa mechi tatu na leo ndio ataanza kutumikia adhabu yake.