Kikosi chetu leo saa 11 jioni kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kikosi kamili na lengo letu la kwanza litakuwa kutafuta pointi tatu.
Alama tatu kwenye mchezo wa leo ni muhimu sana kwetu kwakuwa tunahitaji kurudi katika mbio za ubingwa.
Matola: Tupo tayari kwa Derby…..
Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri na morali zipo juu na tutaingia kwenye mchezo wa leo kwa lengo la kupambana na kupata pointi tatu.
Matola ameongeza kuwa mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani kwa sasa lakini tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunawakabili.
“Kikosi chetu kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo, hii ni Derby na mara zote haijawahi kuwa rahisi. Yanga ni timu bora na kila mtu anajua lakini tupo tayari kuwakabili,” amesema Matola.
Wachezaji wanaitaka ‘Derby’……..
Mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amezungumza kwa niaba ya wachezaji ambapo amesema wao wapo tayari kupambana ili kuwapa furaha mashabiki.
“Sisi kama wachezaji tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho tunajua itakuwa mechi ngumu lakini tutahakikisha tupambana kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki wetu,” amesema Kapombe.