Kikosi chetu leo saa 2:15 usiku kitashuka katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi kuikabili Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-1 tuliopata juzi dhidi ya Singida Fountain Gate.
Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa Mashujaa wanao uonyesha kwa sasa lakini lengo letu ni kuhakikisha tunashinda.
Hali ya timu……
Kocha Msaidizi Seleman Matola amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri na morali zao zipo juu kuelekea mchezo wa leo na anaamini tutazipata pointi zote tatu.
“Ligi inaelekea ukingoni, kila timu inataka kuondoka nafasi iliyopo kujiweka sehemu nzuri zaidi. Tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Mashujaa lakini tumejipanga,” amesema Matola.
Benchikha arejea……
Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha amerejea nchini jana na jioni amekiongoza kikosi kwenye mazoezi ya mwisho yaliyofanyika Uwanja wa Mo Simba Arena.
Benchikha alikwenda nchini Algeria kwa ajili ya kushiriki kozi fupi ya ukocha na atakuwa kwenye benchi kukiongoza kikosi dhidi ya Mashujaa.
Kanoute arejea mzigoni…..
Kiungo mkabaji Sadio Kanoute amepona majeraha yaliyokuwa yanamsumbua na sasa yupo tayari kwa ajili ya mtanange wa leo.
Baada ya takribani wiki mbili Kanoute jana amefanya mazoezi ya mwisho pamoja na wenzake na benchi likiona inafaa wanaweza kumtumia kwenye mchezo wa leo.
Tuliwafunga tulipokutana mara ya mwisho…..
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Februari tatu mwaka huu tuliibuka na ushindi wa bao moja.
Bao hilo lilifungwa na Saido Ntibazonkiza kwa mkwaju wa penati dakika ya 13 baada ya Kibu Denis kufanyiwa madhambi ndani ya 18.