Tunaenda kuandika historia kwa Mkapa leo

Historia mpya ya soka inawekwa leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo kikosi chetu kitakutana na miamba ya Misri, Al Ahly katika uzinduzi wa michuano ya African Football League (AFL) saa 12 jioni.

AFL ni michuano mipya nasisi ndio tumepewa dhamana ya kuifungua kitu ambacho ni heshima na tunaenda kuweka historia leo.

Kitendo cha kupewa heshima ya kuifungua michuano hii nasi tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi katika uwanja wa nyumbani ili kuwapa furaha mashabiki wetu.

Robertinho hana presha na Al Ahly……

Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema ingawa utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora na uzoefu wa Al Ahly lakini hatuna presha.

Robertinho amesema anakiamini kikosi chake, ana matumaini ya kucheza soka safi pamoja na kuibuka na ushindi.

“Sina presha na mchezo wa leo licha yakuwa ni mkubwa, hata mimi nikiwa mchezaji kule Brazil nimewahi kukutana na mechi kama hizi kwahiyo naifurahia na sina presha.”

“Ni mechi kubwa, Al Ahly ni timu bora na ina uzoefu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mpira ni sasa na tupo tayari kwa dakika 90 za kesho,” amesema Robertinho.

Wachezaji wafunguka kuelekea mchezo wa leo…..

Nahodha John Bocco amesema wachezaji wamepata maandalizi ya kutosha kilichobaki ni kufanya mafunzo kwa vitendo uwanjani.

Bocco amesema kila mchezaji ana morali na yupo tayari kupambana kuhakikisha timu inapata ushindi.

“Sisi kama wachezaji tupo tayari kupambana kuhakikisha tunashinda, Al Ahly ni timu bora lakini tupo nyumbani na tunahitaji kuwapa furaha,” amesema Bocco.

Kwa upande wake mshambuliaji Shabani Chilunda amesema “mchezo wa leo ni mkubwa, tunafahamu tutakutana na upinzani mkubwa kutoka kwa Al Ahly lakini tumejiandaa vizuri kuwakabili na kupata ushindi nyumbani.”

Nae mlinzi wa kulia, David Kameta ‘Duchu’ amesema “Sisi kama wachezaji tunafahamu ukubwa wa mchezo huu, tunajua mashabiki wetu watakuja wengi uwanjani na wengine watafuatilia kupitia luninga kwahiyo sisi tumejipanga kuwapa furaha kwa kupata ushindi.”

Inonga ndani……

Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amethibitisha mlinzi wa kati, Henock Inonga atakuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza leo kufuatia kupona majeraha yake.

Uwanja Umejaa wote…..

Mpaka jana mchana tiketi zote zilikuwa zimeuzwa. Tiketi za Platinum ziliisha mapema tu siku mbili baada ya kuanza kuuzwa.

Tumevunja rekodi yetu wenyewe ambayo tuliiweka Agosti, 6 katika Tamasha la Simba Day ambapo tiketi zilimalizika siku moja kabla ya tukio.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER