Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa Uwanja wa Sokoine saa 10 jioni.
Robertinho amesema anawakumbuka vizuri Prisons sababu walitupa upinzani mkubwa msimu uliopita lakini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunawadhibiti.
Robertinho ameongeza kuwa kama kawaida tutaingia kwenye mchezo huo kwa lengo la kucheza soka safi na kupata ushindi.
“Tuna siku moja imebaki ya kufanya mazoezi ili kupata timu ya wachezaji 11 watakaoanza kwenye mchezo wa kesho. Tunategemea kupata upinzani mkubwa.
“Tunawaheshimu Prisons, tunakumbuka msimu uliopita walitupa mechi ngumu lakini tumejipanga, sisi tutaingia uwanjani kwa lengo la kucheza soka safi na kushinda,” amesema Robertinho.
Mlinda mlango, Hussein Abeli amesema kwa upande wa wachezaji kila mmoja yupo tayari kuhakikisha anajitoa kwa kila hali kuhakikisha alama tatu zinapatikana kesho.
“Mara zote tunapokutana na Prisons mchezo unakuwa mgumu, lakini tupo tayari kupambana nao lengo likiwa kuhakikisha tunaondoka na alama tatu,” amesema Abel.