Mtendaji Mkuu wa Klabu, Imani Kajula leo amezindua Programu ya Back to School ambayo itapita mashuleni kwa ajili ya kutafuta mashabiki wapya na kuendeleza vipaji vitakavyoibuliwa.
Kajula amesema huu ni mkatakati ambao utafanyika nchi nzima ambapo Washirika wetu ambao ni Benki za NMB na CRDB wameandaa kadi ambazo zinajulikana kama Simba Caps (Mtoto wa Simba).
Kajula ameongeza kuwa katika mechi zetu mbalimbali tutakuwa na utaratibu wa kualika wanafunzi kutoka shule mbalimbali ili kuzidi kuwandaa watoto ili baadae wajekuwa wahudhuriaji wazuri.
“Tumezindua Programu maalum tuliyoipa jina la Back to School kwa ajili ya kutembelea shule mbalimbali nchi nzima ili kuandaa mashabiki wapya pamoja na kuvumbua vipaji kwakuwa makocha wetu watakuwa wanatembelea huko,” amesema Kajula.
Kwa upande wake Mkuu wa Programu za vijana, Patrick Rweyemamu amesema hii itakuwa sio faida kwa Simba tu bali ni Taifa kwa ujumla kwakuwa tutazalisha wachezaji wengi.
“Programu hii haitakuwa faida kwa Simba pekee bali kwa nchi nzima, tutapita shule mbalimbali na tunaamini tutavumbua vipaji nakuja kuviendeleza,” amesema Rweyemamu.
Mwakilishi wa Benki ya NMB, Hassan Bumbuli ameipongeza Klabu kwa kuona umuhimu wa kutafuta mashabiki wapya wapya watoto kutoka mashuleni huku wakipata kadi za Benki kwa ajili ya maisha yao ya baadae.
“Kipekee niipongeze Simba kwa hili, kuanzia chini kwa watoto ambao wanakuwa wameandaliwa maisha yao ya baadae kwakuwa wamefunguliwa Akaunti za Benki nasi NMB tupo tayari kushiriki kwenye hili,” amesema Bumbuli.