Kocha Mkuu, Didier Gomes Da Rosa amesema mchezo dhidi ya Al Merreikh utakuwa mgumu lakini atatumia mbinu alizotumia katika mechi dhidi ya AS Vita na Al Ahly ili kupata ushindi.
Kocha Gomes amesema atatumia mbinu ya kuzuia kama ilivyokuwa dhidi ya Vita kadhalika na kucheza soka letu la pasi na kutumia vizuri nafasi zitakazopatikana kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa Al Ahly.
Gomes raia wa Ufaransa amesema anaifahamu vizuri Merreikh kwani amewahi kuifundisha kabla ya kujiunga nasi ila anaamini mchezo utakuwa mgumu.
“Itakuwa mechi ngumu, naijua vizuri Al Merreikh kwa hiyo tunawaheshimu lakini tupo tayari kupambana na kuzuia kama tulivyofanya kwa AS Vita na kucheza mpira wetu kama tulivyofanya kwa Al Ahly,” amesema Gomes.
Katika mchezo wa kesho, tunaingia tukiwa vinara wa Kundi A baada ya kushinda mechi mbili dhidi ya Vita na Ahly.