Mtendaji Mkuu wa klabu, Imani Kajula amemtangaza Patrick Rweyemamu kuwa Mkuu wa Programu za soka la vijana katika klabu na Seleman Matola kuwa kocha mkuu.
“Ilikuwa na timu imara lazima uwe na soka la vijana imara, hii sio mara ya kwanza kwa Simba kufanya hivi, tuliwahi kufanya hivyo miaka ya nyuma sasa tunarudi tena.
“Nitangaze rasmi mbele yenu Wanahabari kuwa Patrick Rweyemamu ndiye Mkuu wa programu za timu za vijana na Seleman Matola ni kocha mkuu,” amesema Kajula.
Kwa upande wake Rweyemamu baada ya kutangazwa amesema yeye na Matola wana uzoefu katika kuzalisha wachezaji vijana na anaamini kipindi hiki kutakuwa bora zaidi ya mwanzo.
“Hakuna timu hapa nchini ambayo haina mchezaji ambaye hajapita kwenye mikono ya Simba. Tutaangalia takwimu rasmi lakini zaidi ya wachezaji 250 wamepita Simba.
“Kikubwa tunahitaji kupata ushirikiano, maisha yamepita na vizazi vingine vimezaliwa tunahitaji kuzalisha vipaji vingi zaidi,” amesema Rweyemamu.
Nae Matola ameishukuru Bodi ya Wakurugenzi kwa kuona umuhimu wa kuanzisha programu ya vijana ambazo ndio msingi mkubwa wa mafanikio ya soka kote duniani.
“Naipongeza Bodi kwa kuliona hili, kwetu sio jambo jipya tuliwahi kufanya huko nyuma ila kipindi hiki tutafanya vizuri zaidi kutokana na nguvu kubwa iliyowekwa,” amesema Matola.