Simba Queens imefanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya The Tigers Queens katika mchezo wa Serengeti Lite Women’s Premier League uliopigwa Uwanja wa Uhuru.
Jentrix Shikangwa alitupatia bao la kwanza Dldakika ya 11 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Zainabu Mohamed.
Baada ya bao hilo bado tuliendelea kulishambulia lango la The Tigers ambapo dakika ya 34 Dhanai Bhobho alifunga bao la pili kwa shuti kali alilopiga akiwa kati kati ya uwanja.
Tulienda mapumziko tukiwa mbele kwa mabao 3-0 baada ya Joelle Bukuru kuongeza jingine dakika ya 41 baada ya kupiga mpira wa adhabu uliotinga wavuni moja kwa moja.
Kipindi cha pili tulirudi kwa kasi ambapo dakika ya 47 tulipata bao la nne kupitia kwa Asha Djafar ambaye alimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Mwanahamisi Omari.
Baada ya bao hilo tuliongeza mengine matatu kwa kufuatana dakika za 70, 80 na 90 kupitia kwa Olaiya Barakat, Asha na Amina Ramadhani.
Kocha Charles Lukula alifanya mabadiliko ya kuwatoa Dhanai, Fatuma Issa, Mwanahamisi, Zainabu na Dotto Evarist na kuwaingiza Asha Rashid, Olaiya, Wema Richard, Amina na Diana Mnali.
Ushindi huu unatufanya kufikisha pointi 26 baada ya kucheza mechi 11 tukiendelea kuongoza msimamo wa ligi.