Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ amewaahidi wanachama, wapenzi na mashabiki kuwa kikosi kinaendelea kuboreshwa na mataji ambayo tuliyopoteza tutayarejesha.
Try Again amesema msimu huu tutapambana kuhakikisha tunashinda ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC pamoja na michuano ya Azam Sports Federation Cup ambayo tumefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa hakuna unyonge tena mipango ni thabiti na kila kitu kinaenda sawa huku akigusia suala la usajili la msimu ujao kuwa utakuwa ‘bab kubwa’ na bajeti yake tayari imetengwa.
Try Again amethibitisha kuwa msimu huu tutashiriki michuano ya Super Cup kwakuwa ni miongoni mwa timu bora 10 barani Afrika ambazo ndio zenye vigezo vya kushiriki na hapa nchini tutakuwa timu pekee.
“Tutapambana kuchukua ubingwa wa Ligi pamoja na FC kwa uwezo wa Mungu, na kila kitu kimepangwa na tutafanikiwa.
“Pia kipekee Namshukuru mwekezaji Mohamed Dewji kwa kuendelea kutoa pesa kwa ajili ya kuiboresha timu. Mo anahitaji pongezi kubwa na kwa kiasi kikubwa ameifikisha Simba hapa ilipo.
“Namshuku Mtendaji Mkuu aliyemaliza muda wake Barbara Gonzalez kwa utendaji wake uliotukuka, amefanya kazi kubwa na tunamtakia kila la kheri katika majukumu yake mapya.
“Tutashiriki Super Cup na itakuwa timu pekee kutoka Ukanda huu tupo nafasi 10 kwa ubora Afrika pia hayo ni mafanikio makubwa.” amesema Try Again.