Tumepata pointi tatu kwa KMC Kirumba

Kikosi chetu kimefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Nahodha John Bocco alitupatia bao la kwanza dakika ya 15 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Shomari Kapombe.

Baada ya bao hilo tuliendelea kuliandama lango la KMC huku nao wakitushambulia lakini hata hivyo matokeo hayakubadilika mpaka tunaenda mapumziko.

Sadala Lipangile aliisawazishia KMC bao hilo dakika ya 51 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na kiungo Kenny Ally kufuatia kuwazidi ujanja walinzi wetu.

Augustine Okrah alitupatia bao la pili dakika ya 55 baada ya shuti la Sadio Kanoute kuzuiliwa na mlinda mlango wa KMC, David Kisu.

Dakika ya 73 mlinzi wa kati Henock Inonga alitupatia bao la tatu kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Clatous Chama.

Kocha Juma Mgunda alifanya mabadiliko ya kuwatoa Okrah, Bocco na Pape Sakho na kuwaingiza Kibu Denis, Habib Kyombo na Victor Akpan.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER