Tunashuka kwa Mkapa Leo kuikabili Kagera

Kikosi chetu leo saa moja usiku kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Kagera Sugar.

Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 tuliopata Jumatano dhidi ya Geita Gold kwenye mechi ya kwanza.

Kagera ni moja ya timu ambazo imekuwa ikitupa upinzani mkubwa kila tunapokutana na tunategemea hilo pia kutokea kwenye mchezo wa leo.

MATOLA AELEZEA HALI YA TIMU

Kocha msaidizi Seleman Matola amesema kikosi kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo na wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri.

Matola amesema wachezaji wote wamefanya mazoezi ya mwisho jana na hakuna aliyepata majeraha hivyo hatutamkosa yoyote kwenye mchezo wa leo.

Pamoja nakuwa katika uwanja wa nyumbani Matola amesema tutaingia kwa kuwaheshimu Kagera kwakuwa ni timu nzuri hivyo tutachukua tahadhari zote.

“Kikosi kipo tayari, tunamshukuru Mungu hakuna mchezaji yoyote ambaye tutamkosa kutokana na majeraha au sababu yoyote, tunajua mchezo utakuwa mgumu lakini lengo letu ni ushindi,” amesema Matola.

KAPOMBE AWAITA MASHABIKI

Mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amewaomba mashabiki waje kwa wingi kwa Mkapa kama kawaida yao ili kuwapa hamasa na wao watakuwa na jukumu moja kuhakikisha wanafurahi.

Kapombe amesema kwa upande wao wachezaji watahakikisha wanafuata maelekezo ya walimu ili kuisaidia timu kubakisha alama zote tatu nyumbani.

“Sisi kama wachezaji tupo tayari kwa mchezo wa leo, tumepata maandalizi mazuri kutoka kwa walimu wetu kikubwa tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani tunaamini tutawapa furaha,” amesema Kapombe.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER