Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa 12 jioni kuikabili Geita Gold katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC 2022/23.
Tumejipanga kuhakikisha tunarejesha mataji yote tuliyopoteza msimu uliopita kwa hiyo tunahitaji kushinda kila mchezo.
Geita ni timu nzuri na inacheza kitimu tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini tumejipanga kuhakikisha tunabakisha pointi zote tatu katika Uwanja wa nyumbani.
KOCHA ZORAN ATOA NENO
Kocha Mkuu Zoran Maki amesema timu haijapata maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo wa leo baada ya kucheza mechi ngumu ya Ngao ya Jamii Jumamosi.
Amesema baada ya mechi ya Jumamosi wachezaji walipewa mapumziko ya siku moja kisha Jumatatu na Jumanne ndiyo tulifanya mazoezi kamili hivyo hayajatosha kuelekea mchezo wa leo.
Hata hivyo, Kocha Zoran ameongeza kuwa licha ya hayo tumejipanga kuhakikisha tunapambana kushinda ili kubakisha alama tatu nyumbani.
“Wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo wa kesho, itakuwa jambo zuri kuanza kwa ushindi ingawa tunafahamu itakuwa mechi ngumu.
“Geita imemaliza nafasi ya nne msimu uliopita nasi ya pili kwa hiyo inaonyesha zinakutakana timu mbili bora, ushindani utakuwa mkubwa lakini tumejipanga kwa ushindi,” amesema Kocha Zoran.
KAPOMBE AFUNGUKA
Mlinzi wa kulia Shomari Kapombe amesema kwa upande wa wachezaji wapo kwenye hali nzuri na tayari kwa mchezo na kila mmoja lengo lake ni ushindi.
“Geita ni timu nzuri na imekuwa ikitupa upinzani mkubwa kila tukikutana nao, tunajua pia msimu huu watashiriki Kombe la Shirikisho Afrika hivyo wanahitaji kufanya vizuri lakini tumejipanga kushinda,” amesema Kapombe.
HALI YA KIKOSI
Kocha Zoran amesema wachezaji wote ambao tumewasajili kwa ajili ya msimu huu wa ligi 2022/23 wapo fiti tayari kwa mchezo wa leo na hakuna ambaye atakosekana kwa sababu yoyote.