Kocha Msaidizi, Seleman Matola ameweka wazi kuwa pamoja na ubora walionao Singida Black Stars tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda mchezo wa kesho na kutinga fainali ya CRDB Federation Cup.
Matola amesema haitakuwa mechi rahisi hasa ukizingatia siku mbili zilizopita tumetoka kucheza nao na kushinda kwa bao moja hivyo watakuja kwa nia ya kulipa kisasi lakini tupo tayari kuwakabili.
Akizungumzia hali ya kikosi, Matola amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na hakuna aliyepata majeraha ambayo yatamfanya kuukosa mchezo wa kesho.
“Tunamshukuru Mungu tumefika salama Manyara, kikosi kipo kwenye hali nzuri kwa ajili ya kupambana muda wote ili kupata ushindi umuhimu, tunaiheshimu Singida na tunategemea kupata upinzani mkubwa.”
“Tunajua Singida watakuja tofauti na walivyokuja juzi lakini malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda na kutinga fainali,” amesema Matola.
Kwa upande wake nahodha wa timu Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema ratiba ni ngumu kwa upande wetu kutokana na kucheza mechi karibu karibu lakini hata hivyo tupo tayari kuhakikisha tunashinda na kutinga fainali.
“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kwa ajili mchezo wa kesho, hakutakuwa na tofauti kubwa kwakuwa tumecheza dhidi yao siku mbili zilizopita ila malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda na kutinga fainali,” amesema Zimbwe Jr.