Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa KMC Complex kuikabili Dodoma Jiji katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo huu ni wa kiporo kwakuwa awali ulipangwa kuchezwa Februari 15 lakini basi la Dodoma Jiji lilipata ajali Wilayani Ruangwa mkoani Lindi wakati likija Dar es Salaam hali iliyofanya kuahirishwa kwa mechi hiyo.
Maandalizi ya mchezo yamekamilika na malengo yetu ni kuhakikisha tunaendeleza kampeni yetu ya kushinda mechi zote 10 zilizokuwa zimebaki kabla ya kumalizika kwa msimu.
Kauli ya benchi la ufundi….
Kuelekea mchezo wa leo kocha msaidizi, Seleman Matola amesema utakuwa mchezo mgumu wenye ushindani mkubwa lakini tumejiandaa kuhakikisha tunatumia vizuri nafasi tutakazozipata na kuzifanya mabao.
Matola amesema haiwezi kuwa mechi rahisi kwakuwa hata Dodoma wanahitaji alama tatu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo lakini tumewaandaa wachezaji vizuri kuhakikisha tunapata matokeo chanya.
“Haiwezi kuwa mechi rahisi Dodoma wana timu nzuri na mwalimu anayependa ushindani, kikosi chetu kipo tayari kwa kupambana hadi mwisho kutafuta alama tatu muhimu.
“Malengo yetu yanabaki kuwa yale yale ya kushinda kila mchezo, tunajua itakuwa mechi ngumu hasa kwakuwa tunaelekea mwishoni mwa msimu lakini tupo tayari,” amesema Matola.
Wachezaji wapo tayari kwa vita ya dakika 90…….
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia David Kameta ‘Duchu’ amesema kwa upande wao wapo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha ushindi unapatikana na kuwapa furaha Wanasimba.
“Tunaijua vizuri Dodoma Jiji, ni timu imara lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo chanya, kwetu kila mchezo ni fainali na malengo yetu ni kupata ubingwa msimu huu,” amesema Duchu.
Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza…..
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Septemba 29, 2024 tuliibuka na ushindi wa bao moja.
Bao hilo lilifungwa kwa mkwaju wa penati na Jean Charles Ahoua kufuatia nahodha Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ kufanyiwa madhambi ndani ya 18 na kiungo Salmin Hoza.
Kapombe kuikosa Dodoma…..
Mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe hatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.