Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili CS Sfaxien kutoka Tunisia katika mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ni mechi ya tatu ya hatua ya makundi pia ni mchezo wa pili wa nyumbani hivyo tunaamini utakuwa mchezo mgumu na tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi zote tatu.
Tunahitaji kushinda na kuonyesha soka safi katika mchezo wa leo ili kuwafurahisha mashabiki ambao tunaamini watakuja kwa wingi uwanjani.
Maneno ya Kocha Fadlu Davids….
Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema mchezo dhidi ya CS Sfaxien utakuwa mgumu kwakuwa kila timu inahitaji kupata pointi ili kujiweka sehemu salama zaidi lakini tupo nyumbani na tuna faida yakuwa na mashabiki wetu.
Fadlu ameongeza kuwa kikosi kipo kwenye hali nzuri na wachezaji wapo tayari kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu nyumbani.
“Kikosi chetu kipo kwenye hali nzuri kwa ajili ya mchezo wa leo, jana tumefanya mazoezi ya mwisho na wachezaji wapo kweli hali nzuri tayari kwa mechi ambayo tunaamini itakuwa ngumu lakini tumejipanga kupata matokeo chanya,” amesema Kocha Fadlu Davids.
Wachezaji wanaitaka mechi……
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo mkabaji, Augustine Okajepha amesema kwa upande wao wapo tayari na kila atayepata nafasi amejipanga kufanya vizuri ili kuwapa furaha Wanasimba.
“Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu lakini tumejiandaa kupambana mpaka mwisho kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema Okajepha.
Hatujawahi kukutana na CS Sfaxien…
Licha ya kwenda mara kadhaa Tunisia kucheza mechi kwenye michuano hii na timu za kule kuja nchini lakini tulikuwa hatujawahi kukutana na CS Sfaxien na leo ni mara ya kwanza.
Hali ya Kikosi….
Wachezaji wetu ambao walikuwa majeruhi wamerejea kikosini hivyo Kocha Fadlu Davids na wasaidizi wake watakuwa na wigo mpana wa kuchagua na kupanga kikosi kwenye mchezo wa leo.